Dunia
ya Watoto
Idhaa hii ya Kiswahili ya BBC, London ikishirikiana na Shirika la Kimataifa la
Kuhudumia Watoto, UNICEF inakuletea sauti za watoto wakielezea juu ya ndoto
zao, furaha na vicheko vyao, vilio na huzuni zao, malalamiko, mafanikio
matumaini na matarajio yao ya karne hii ya 21.
Vipindi hivi vilitangazwa kwa mara ya kwanza katika Idhaa hii wakati wa
kusherehekea miaka 10 ya Haki za Mtoto Duniani.
Haki
za Mtoto
Katika mfululizo wa makala hizi 10 tutaweza kufahamu ni jinsi gani wazazi,
serikali na mashirika katika nchi hizo zimeweza kuzingatia mkataba huo na
kuheshimu haki hizo. Mada zetu ni pamoja na Haki ya Elimu, Watoto na Ajira,
Elimu ya Uhusiano wa wasichana na wavulana, Mahojiano ya Watoto na Rais, na
Matarajio yao katika Karne ijayo.
Hali halisi
Akishirikiana na UNICEF, Vicky Ntetema, mwandishi wa Habari na mtayarishaji wa
vipindi hivi alitembelea Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Rwanda, Burundi,
Uganda, Kenya na Tanzania ili kuzungumza na watoto na kujionea hali halisi ya
watoto katika nchi hizo. Msimulizi wako ni Maria Kitambi.
Makala ya Kwanza: Afya Bora
Katika Makala hii ya Kwanza tutaanza kwa kuangalia juu ya Haki za Mtoto na
kisha utasikia wataalamu wakizungumzia juu ya masuala muhimu katika kulinda
Afya ya mtoto.
Vile vile viongozi wa UNICEF na serikali watazungumzia juu ya mafanikio katika
utekelezaji wa baadhi ya haki hiyo ya kumpatia mtoto huduma bora ya Afya.
Makala ya Pili: Matunzo Bora
Wiki iliyopita ulisikia juu ya Haki ya Mtoto ya Afya Bora na umuhimu wa chanjo
kwa watoto. Juma hili tunazungumzia juu ya Haki ya Matunzo Bora.
Mkataba wa Haki ya Mtoto unasema kwamba Maendeleo ya mtoto yanahusu ukuaji wake
kimwili, kiakili, kimaadili na kiroho.
Makala ya Tatu: Haki ya Elimu
Wiki hii Dunia ya Watoto inaangalia juu ya Haki ya Elimu. Ripoti ya UNICEF ya
Maendeleo ya Mataifa inasema kwamba zaidi ya watoto milioni 130 duniani wenye
umri wa kwenda shule za msingi, hawapo mashuleni.
Kiasi kikubwa ni wasichana ambao wananyimwa haki ya elimu na hivyo kunyimwa
haki ya kuwa na maisha mazuri baadaye. Makala hii inadhihirisha jinsi gani
watoto wanavyoathirika na ukiukaji wa utekelezaji wa Haki hiyo ya Elimu.
Makala ya Nne: Haki ya Elimu ya Jamii
Juma hili Dunia ya Watoto inaangalia juu ya HAKI YA ELIMU ya Jamii katika
jitihada za kuepusha maradhi ya zinaa kwa watoto na pia mimba kwa wasichana
wenye umri mdogo.
Je, serikali zinachukua hatua gani ili kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya
unyanyaswaji wa kijinsia, ukahaba, maandishi, picha au filamu zinazohusu zinaa?
Na Mkataba wa Kimataifa wa Haki ya Mtoto Duniani unazungumzia nini juu ya mila
na desturi potofu zinazoendekeza vitendo vya dhuluma na ukatili dhidi ya mtoto
vinavyoathiri utu wake na afya yake?
Makala ya Tano: Athari za Tohara
Wiki hii tunaangalia zaidi athari za Tohara kwa wasichana na vile vile madhara
ya UKIMWI kwa watoto. Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto unasisitiza juu ya
kuzingatia mila na desturi nzuri katika kusaidia malezi mema ya kimwili,
kiakili, kiroho na kimaadili kwa mtoto.
Jinsi gani mafunzo ya Tohara kwa wasichana yanaweza kutumika katika kumlinda
mtoto? Je watoto wenyewe, wazazi na walezi wana mtizamo gani kuhusiana na suala
mila hii na nyinginezo ambazo ni potofu?
Makala ya Sita: Kazi za Sulubu kwa WatotoZaidi ya miaka 10 imepita sasa
tangu Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto ulipotiwa saini na bado jamii
kadhaa zinashindwa kutekeleza haki hizo na hivyo kuwafanya watoto kuwa na
maisha magumu zaidi.
Je karne hii itamkuta mtoto katika hali gani? Katika makala hii tunasikia jinsi
gani watoto wanajikuta wakifanya kazi za sulubu na vibarua kandamizi na hata
kuingia katika shughuli za ukahaba.
Makala ya Saba: Watoto kwenye Mazingira Magumu
Katika makala hii tunazungumza na watoto wanaoishi kwenye Mazingira Magumu.
Watoto hao hawataki kuitwa watoto wa mitaani kwani wanasema wamezaliwa na
wazazi waliokuwa katika kaya zao.
Vile vile wanatoa ushauri kwa watoto wengine ili wasije wakatumbukia kwenye
mitego mibaya na vile vile jinsi gani wanaweza kujikwamua kutoka katika hali
hiyo ngumu. Kwa jinsi gani upendo ndani ya nyumba unaweza kuchangia katika
kutatua suala kama hilo kwa watoto.
Makala ya Nane: Watoto Wahalifu
Makala ya juma hili yanahusu Watoto Wahalifu. Kwa nini watoto wanajikuta
mahabusu kutokana na vitendo vinavyokiuka sheria?
Je, walezi wa watoto waliopo mahabusu na kwenye vituo vya kuwarekebisha watoto
wanachukua hatua gani kuhakikisha kwamba watoto hao wakitoka huko wanawezaje
kurudi katika jamii na kujiendeleza?
Makala ya Tisa: Watoto wamhoji Rais Mkapa wa Tanzania
Juma hili sikiliza jinsi historia ya watoto wa Tanzania ilivyojiandika baada ya
kuwakilisha matatizo yao kwa Rais wao, Bwana Benjamin Mkapa.
Vile vile hii ni mara ya kwanza kabisa katika historia ya matangazo ya BBC kwa
watoto mbali mbali kufanya mahojiano ya ana kwaa ana na kiongozi wao wa taifa.
Makala ya Kumi: Ndoto na Matarajio ya Watoto
Katika makala hii watoto wanatuelezea juu ya ndoto zao na matarajio yao katika
maisha. Wanatamka wazi wazi juu ya mwelekeo wanaotaka kuuchukua ili kufikia
malengo waliyoyapanga na jinsi gani jamii, serikali, wazazi na walezi wanaweza
kuwasaidia ili kukamilisha ndoto zao.
Vipindi hivi vya Dunia ya Watoto vimetolewa kwa ushirikiano wa Shirika la
Utangazaji la BBC na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Watoto, UNICEF,
vimetayarishwa na Vicky Ntetema (Mwandishi wa Habari na Mtangazaji wa Idhaa ya
Kiswahili) na kuletwa kwako na Maria Kitambi.
Kwa maelezo zaidi kuhusiana na vipindi hivi na jinsi gani unaweza kupata
kijitabu cha Haki za Mtoto duniani, wasiliana na:
swahili@bbc.co.uk au
vicky.ntetema@bbc.co.uk
Vile vile unaweza kupata maelezo zaidi kuhusiana na Haki ya Mtoto chini ya
Mkataba wa Kimataifa katika ofisi za UNICEF zilizopo karibu na mahali ulipo
(Bujumbura, Dar es Salaam, Kampala, Kigali, Kinshasa na Nairobi).